Wana wa Israeli walipokaribia mwisho wa miaka yao 40 ya kutangatanga jangwani na walipokuwa karibu kuingia Kanaani, Yoshua aliyekuwa akiwaongoza alipokea ujumbe ufuatao kutoka kwa Mungu:
Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda kulingana na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kulia, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. (Yoshua 1:7).
Unaelewaje maagizo haya? Unaposikia mwito wa kutii sheria ya Mungu, nini huja akilini mwako? Je, unafikiria sheria ya Mungu kama sheria za kibinadamu — kanuni zinazowekwa ambazo Mungu huzisimamia na kutekeleza kwa adhabu? Au unafikiria sheria ambazo Muumba aliweka katika utendaji wa uhalisia — sheria za fizikia, mvuto (gravity) , afya, na sheria za maadili?
Je, unasikia mwito wa Mungu wa utii kama vile mwito wa daktari wa kuishi kwa afya (katika mwafaka na sheria za afya), au unasikia mwito wa Mungu wa utii kama onyo la askari polisi la kutokukimbiza gari kwa mwendo kasi?
Ni ukweli wa kusikitisha wa historia kwamba sehemu kubwa ya Ukristo imekubali uongo kwamba sheria ya Mungu hufanya kazi sawa tu na sheria za wanadamu—kanuni zilizobuniwa na kutekelezwa kwa adhabu. Lakini hebu tuchunguze utii unaotokana na sheria, kanuni, vitisho vya adhabu, na utekelezaji wa sheria—ukilinganisha na utii unaotokana na upendo, uaminifu, ambao pia hujulikana kama imani. Kisha tuchunguze jinsi upendo na uaminifu vinavyopandwa katika mioyo na akili na kupelekea utii.
UTII WA SHERIA
Fikiria umesimama chini ya msalaba wakati Yesu anasulubiwa. Unazungumza na Kayafa na viongozi wengine wa dini ya Kiyahudi wanaomdhihaki, kumtesa, na kumsulubisha Kristo. Unadhani wangetoa majibu gani kwa maswali yafuatayo?
- Je, ni muhimu kuwa na utii wa agano kwa Mungu? “Kabisa!” naweza kuwasikia wakisema, “Tunaishi kwa ili kutii agano—sisi sote tumetahiriwa ipasavyo kama agano linavyoagiza.”
- Je, ni muhimu kuitii sheria ya Mungu? “Bila shaka. Na kama hawa wahalifu hawatakufa upesi, tutamwomba Pilato aharakishe vifo vyao ili tuweze kuitunza Sabato kulingana na sheria.”
- Je, ni muhimu kuitii sheria ambayo Musa mtumishi wa Mungu alitupa? “Bila shaka! Maisha yetu yote tunaishi tukilenga kutii sheria hiyo.”
Na kama tungewauliza, “Kwa nini mnamsulubisha huyu mtu?” naweza kuwasikia wakijibu:
“Naam, umeshatueleza wewe mwenyewe—lazima tuwe watiifu kwa agano, lazima tutii sheria ya Mungu, lazima tutii sheria ambazo Mungu alitupatia kupitia Musa—na huyu mtu anazivunja mara kwa mara. Musa alituagiza tumpige kwa mawe mzinzi, lakini huyu mtu aliwasamehe. Musa alitupa ruhusa ya kuwataliki wake zetu, lakini huyu mtu alisema tusifanye hivyo. Musa alitufundisha tusifanye kazi siku ya Sabato, lakini huyu mtu aliwaponya wagonjwa siku ya Sabato na wanafunzi wake walivuna punje siku ya Sabato. Musa alitufundisha kuosha kwa namna fulani kabla ya kula, lakini huyu mtu hakuwaelekeza wanafunzi wake wafanye hivyo. Musa alitufundisha kwamba sheria lazima zitekelezwe na kwamba uovu lazima uondolewe katika jamii, na ndicho tunachofanya kwa sababu sisi ni watoto wa Abrahamu na wa Mungu, na tumejitoa kwa uaminifu na utii wa agano.”
Utii wa sheria na utekelezaji wa sheria hauna uwezo wa kubadili mioyo na akili, wala kusimika upendo, uaminifu, urafiki, uaminifu wa kudumu, na kujitoa. Utii wa uongozi wa Kiyahudi uliomsulubisha Kristo ulikuwa aina iliyowafanya wawe maadui wa Mungu huku wakidai kuwa watoto wake na kufanya kazi yake.
Mtume Paulo anashughulikia mwelekeo huu wote wa kisheria usio sahihi kuhusu utii katika kitabu cha Warumi, na analinganisha utii unaotokana na sheria na utii unaotokana na imani au uaminifu. Anaanza kitabu cha Warumi kwa kusema:
Kupitia yeye na kwa ajili ya jina lake, tumepokea neema na utume ili kuwaita watu kutoka mataifa yote katika utii unaotokana na imani. (Warumi 1:5).
Imani au uaminifu si kitu kinachoweza kuamriwa, kutungwa kwa sheria, kuagizwa, au kupatikana kwa njia ya sheria na utekelezaji wake. Uaminifu hujengwa juu ya uaminifu halisi wa maisha, unaohitaji ushahidi, ambao lazima ueleweke na kuishiwa. Uaminifu hauwezi kuanzishwa kwa tangazo, madai, amri, maagizo, kanuni, na masharti, na utadhoofishwa na vitisho na adhabu. Jaribu kupata uaminifu wa mtu kwa kumtishia kumdhuru au kumwadhibu ikiwa hatakuamini—haiwezekani kabisa! Sheria zilizolazimishwa na utekelezaji wake haziwezi kuvutia mioyo na akili, na hatimaye, zitawageuza wale wanaotumia mbinu hizo kama njia ya kutafuta haki kuwa waasi.
Paulo, akielewa hili, baada ya kutufundisha kwamba anawaita watu kwenye utii unaotokana na imani, anatueleza msingi wa imani hiyo. Katika Warumi 1:20 anaandika:
Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, sifa zisizoonekana za Mungu—uwezo wake wa milele na asili yake ya uungu—zimeonekana wazi, zikieleweka kutokana na mambo yaliyoumbwa, hivyo watu hawana udhuru (NIV msisitizo wangu).
Imani yetu kwa Mungu haijengwi juu ya madai, maneno, au amri, bali juu ya uhalisia, ushahidi, na ukweli. Mungu ni Muumba, na sheria zake ndizo sheria zinazoongoza jinsi uhalisia unavyofanya kazi. Paulo anatufahamisha kwamba ufalme wa Mungu ni ufalme wa uhalisia—sheria za milele za muundo (design laws) zinazoongoza shughuli za asili—na kwa hiyo ufalme wa Mungu haufanyi kazi kwa kanuni zilizobuniwa zinazohitaji adhabu za nje kama viumbe hufanya.
Paulo anaendelea kusema kwamba watu ambao hawajaletewa Neno la Mungu lililoandikwa, lakini wanaelewa uhalisia wa ufalme wa Mungu wa ukweli, upendo, na uhuru unaofunuliwa kupitia sheria za ubunifu wa uumbaji zilizojengwa katika asili, na hivyo kuchagua kumwamini, hupokea moyo mpya na roho iliyo sahihi, na sheria ya Mungu huandikwa mioyoni mwao. Wanakuwa washiriki wa agano jipya la wokovu (Waebrania 8:10).
“Wote watendao dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, na wote watendao dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria [Torati]. Kwa maana si wale wanaosikia sheria ndio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaotii sheria atakaotangazwa kuwa wenye haki. (Hakika, watu wa mataifa, wasio na sheria, wanafanya kwa asili mambo yanayotakiwa na sheria, wao wenyewe ni sheria kwao, ingawa hawana sheria, kwa kuwa wanaonyesha kwamba matakwa ya sheria yameandikwa mioyoni mwao, dhamiri zao zikiwa mashahidi, na mawazo yao mara nyingine yakiwashitaki, mara nyingine hata yakiwatetea.)” (Warumi 2:12–15, NIV84, msisitizo wangu).
Paulo anaeleza uhalisia kwamba sheria za ubunifu wa Mungu zimejengwa ndani ya jinsi uhalisia unavyofanya kazi. Hata kama hakuna mtu anayekufundisha shuleni, wala husomi katika kitabu, lakini unazitambua katika asili na kuishi kwa upatanifu nazo kwa sababu unazithamini na kuzichagua, basi umechagua kumwamini Muumba, na Roho Mtakatifu hufanya kazi moyoni mwako kuandika sheria yake ndani yako. Kupitia ushindi wa Kristo, Roho Mtakatifu huleta maisha ya Kristo—ya ukweli, upendo, na uhuru—sheria za ubunifu wa Mungu—na kuzizalisha katika akili na moyo wako; huo ndio uzoefu wa agano jipya. Hata kama mtu bado hajasikia jina la Yesu, bado anaokolewa naye kwa sababu Yeye ni Muumba na Mtegemezaji wa asili. Uponyaji huu, mabadiliko, urejesho wa moyo na akili hauwezi kufanywa kwa njia za kisheria za nje.
Kuwa makini na kile Paulo anaandika baadaye:
Basi wewe unayejiita Myahudi; unayelitegemea torati na kujisifu kwa uhusiano wako na Mungu; unayejua mapenzi yake na kuidhinisha yaliyo bora kwa kuwa umefundishwa na torati; unayejiaminisha kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, nuru kwa walio gizani, mwalimu wa wapumbavu, mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una umbo la maarifa na ukweli katika torati—wewe basi unayefundisha wengine, hujifundishi? Wewe uhubiriye usiibe, waiba? Wewe usemaye watu wasizini, wazini? Wewe uchukiaye sanamu, waibia mahekalu? Wewe ujisifuye kwa torati, wamheshimu Mungu kwa kuivunja torati? Kama ilivyoandikwa: “Jina la Mungu linakufuriwa kati ya Mataifa kwa sababu yenu.” (Warumi 2:17–24 NIV).
Paulo anakabiliana na njia ya utii inayotegemea sheria zilizowekwa kwa nguvu, dini ya kisheria, na kutunza kanuni. Hii ni sawa na kuwaambia madaktari:
“Enyi mnaojiita viongozi wa huduma ya afya, mnaotegemea maarifa ya vitabu vyenu vya udaktari na kujisifu kwamba mna elimu zaidi; mkijiona kuwa waongoza wagonjwa kwa sababu mna vitabu—mbona hamjifundishi kuishi kwa afya? Kwa nini hamwachi kuvuta sigara? Kwa nini hamwachi kunywa pombe? Kwa nini hampati saa nane za usingizi kila usiku? Ninyi mnaochukia magonjwa kwa wengine na kujisifu kwa utaalamu wenu, kwa nini mnamdharau Mungu kwa kuvunja sheria zake za afya kwa jinsi mnavyoishi? Kama ilivyoandikwa, Mungu anawakilishwa vibaya kwa sababu yenu.”
Baada ya Paulo kuwaonya kwa kuwa na mtazamo wa kisheria wa dini huku wakiishi kinyume na sheria za ubunifu was Mungu katka uumbaji, anaandika:
Kwa kweli, Mataifa wasiotahiriwa wanaoitunza sheria ya Mungu watawahukumu ninyi Wayahudi mliotahiriwa na mnao torati lakini hamtiii (Warumi 2:27 NLT).
Paulo anasema kwamba wale ambao hawajawahi kwenda shule ya udaktari lakini wanaishi kwa upatanifu na sheria za afya za Mungu watawahukumu madaktari walio na vitabu lakini wanavunja sheria za afya.
Kisha anaeleza kwamba tohara si ya kisheria, ya tabia, au ya nje, bali ni tohara ya moyo kwa Roho—uhalisia—kukata roho ya hofu na ubinafsi na kuanzisha utambulisho wetu juu ya Roho Mtakatifu wa Mungu – maisha ya Kristo, roho ya upendo na uaminifu, inayoturejesha katika upatanifu na sheria za muundo za Mungu kwa maisha.
Paulo anaendelea kusisitiza kwamba sheria zilizowekwa kwa nguvu, dini ya kisheria, na utendaji wa nje havina nguvu ya kuokoa. Wokovu ni uhalisia wa Yesu kurejesha sheria yake hai ya upendo ndani ya ubinadamu. Katika Warumi 3 tunasoma:
Lakini sasa Mungu ameifunua hali ya afya ya ndani—tabia iliyo sawa na kamilifu kwa kila njia—ambayo haikutokana na maandiko ya kisheria, bali ndiyo ile ambayo Maandiko na Amri Kumi zilikuwa zikielekeza akili zenu. Hali hii kamilifu hutoka kwa Kristo na huumbwa ndani yetu na Mungu tunapomwamini. Uaminifu wetu kwake huanzishwa kwa ushahidi uliotolewa kupitia Yesu Kristo wa uaminifu wake wa juu kabisa. Hakuna tofauti kati ya makabila, kwa maana wanadamu wote wameambukizwa ugonjwa ule ule—wa kutoamini, hofu, na ubinafsi—na wamepotoshwa katika tabia na kukosa sana kiwango cha utukufu wa Mungu kwa ubinadamu. Hata hivyo, wote walio tayari huponywa bure kwa Dawa ya neema ya Mungu iliyotolewa na Yesu Kristo. Mungu alimtoa Yesu kama njia na chombo cha urejesho. Sasa, kupitia uaminifu uliowekwa kwa ushahidi wa tabia ya Mungu uliofunuliwa Kristo alipokufa, tunaweza kushiriki Dawa hiyo iliyopatikana kwa njia ya Kristo. Mungu alifanya hivi kuonyesha kwamba yeye ni wa haki na mwema—kwa maana kwa uvumilivu wake alisimamisha kwa muda matokeo ya mwisho ya kutokuwa katika upatanifu na muundo wake wa maisha—ingawa ameshtakiwa kwa uongo kuwa si wa haki. Alifanya hivi kuonyesha kwa wakati huu jinsi alivyo wa haki na mwema, ili aonekane kuwa wa haki anapowaponya wanaomwamini Yesu. (Warumi 3:21–26 Remedy).
Paulo anaendelea na hoja hii katika Warumi, lakini tukiruka hadi sura ya 14, anahitimisha tatizo kuu la dhambi:
Kila kisichotokana na imani ni dhambi (Warumi 14:23 NIV).
Hili ndilo tatizo, swali husika, kiini cha wokovu. Kwa msingi wake, dhambi ni kutomwamini Mungu. Adamu na Hawa walimkosa Mungu kwa kutoamini, na kutoamini kwao kulibadilisha roho yao kutoka upendo na uaminifu kwenda hofu na ubinafsi. Hofu na ubinafsi husababisha watu kutenda ili kujilinda na kujikuza—ambayo ni kinyume cha upendo.
Kwa sababu ya dhambi ya Adamu, tunazaliwa na roho ya hofu na ubinafsi, na wokovu unahitaji tuzaliwe upya kwa Roho/uzima wa Yesu—roho ya upendo na uaminifu. Hili haliwezi kutimizwa kwa sheria zilizowekwa kwa nguvu na utekelezaji wake. Kwa kweli, sheria zilizowekwa kwa nguvu huongeza hofu na kupunguza uaminifu na upendo. Uongo kwamba sheria ya Mungu hufanya kazi kama sheria za kibinadamu husababisha dini za kisheria kama ile ya Wayahudi waliomsulubisha Kristo; lakini wokovu unahitaji kuzaliwa upya.
Utii anaoutamani Mungu si kufanana kwa tabia ya kutunza kanuni, bali ni utii wa marafiki wanaopenda, mioyo yao imebadilishwa kutoka kutoamini, hofu, na ubinafsi kwenda ukweli, upendo, na uaminifu. Hili hutimizwa tu kwa njia za Mungu za ukweli na upendo; ndiyo maana Biblia inasema:
“Si kwa nguvu wala kwa uwezo, bali kwa Roho yangu,” asema BWANA wa majeshi (Zekaria 4:6 NIV).
Mungu hawezi kushinda, wala kurejesha upendo na uaminifu mioyoni na akilini kwa kutumia nguvu na uwezo; hufanya hivyo kwa Roho wake wa ukweli na upendo.
Utii wa kweli ni utii unaochipuka kutoka kwa upendo na uaminifu kwa Mungu, unaotoka katika moyo uliozaliwa upya na unaochochewa na Roho wa Kristo.
Nakuhimiza ukatae uongo kwamba sheria ya Mungu hufanya kazi kama sheria za kibinadamu, na urejee kumwabudu Mungu kama Muumba, ukitambua kwamba sheria zote za Mungu ni sheria za ubunifu wa uumbaji zilizojengwa ndani ya jinsi uhalisia unavyofanya kazi. Kisha, kama bado hujafanya hivyo, fungua moyo wako kwake na uzaliwe upya katika uzima tele ambamo utii wa kweli unawezekana—utiifu wa upendo na uaminifu!











using your credit or debit card (no PayPal account needed, unless you want to set up a monthly, recurring payment).
instead?